Desemba na Januari imekuwa miezi ya pilikapilika sana katika mtandao wetu, na mengi yametokea. Natamani ningelikuwa Dar nipate kuongea nanyi ana kwa ana, lakini kwa vile hilo haliwezekani imenipasa kuandika barua ambayo itatafsiriwa na kuchapishwa na Donatian ili kila mmoja wenu apate nakala.
Kwa vile huu ni mwaka mpya, ningependa kuanza kwa kuwakumbushia sababu za shirika letu huku London kufadhili mtandao wenu.
Kwa nini tunawafadhili ninyi
Sababu yetu ya kwanza ni kwamba tunataka kusaidia watoto wa Afrika wanaoishi katika mazingira magumu zaidi. Sababu yetu ya pili ni kwamba tunataka kuwahakikishia wafadhili wengine kwamba Asasi ndogondogo za kijamii(CBO) zinaweza kuwajibika vizuri zaidi kuliko Asasi kubwa zisizo za kiserikali (NGO). Wafadhili wengine wanadhani kwamba wakifadhili Asasi ndogondogo zitafuja fedha hizo. Tunataka tuwathibitishie kwamba hiyo ni fikra potofu, kwani Asasi ndogondogo zinaweza kutumia fedha zitolewazo kwa busara zaidi. Endapo tutafanikiwa kuthibitisha hili, basi wafadhili wengine wataweza pia kutupatia fedha zaidi ili tuweze kufadhili mitandao mingi zaidi katika miji mingine mingi.
Viongozi wapya
Kama mnavyofahamu, tumeishapata viongozi wapya wa mtandao na nina imani kwamba Jaka, steven na Shabani watafanya kazi nzuri sana. Kwa vile ndo wanaanza tu, kumekuwepo na matatizo katika mahusiano miongoni mwao. Ninaweza kuelewa kwamba viongozi wapya wanayo nia njema, na wako makini kutuonyesha katika shirika letu huku London kwamba waanafanya kazi barabara na wanakubali changamoto. Hata hivyo, tulitegemea mapungufu yangelijitokeza mwanzoni, na hilo sio tatizo; mategemeo yetu ni kwamba kadri muda utakavyoenda ndivyo viongozi watakavyo zidi kuwa na ufanisi zaidi. Nasi pia tunatarajia kwamba viongozi hawa wataweza pia kufanya kazi kwa pamoja kwa amani na utulivu zaidi.
Ziara za vikundi kwa mwezi Desemba
Nilipotembelea vikundi wakati wa mwezi Desemba, hapa kuna baadhi ya vitu nilivyokuta:
* Katika kikundi kimoja, hakukuwa na uthibitisho wowote ule kwamba fedha zetu zimetumika kuwasaidia watoto. Kikundi kiliandika kumbukumbu za mahesabu siku chache kabla ya safari yetu kuelezea namna kilivyotumia fedha, lakini hapakuwa na risiti. Na kulikuwa na dalili kwamba fedha ziliibiwa: mwanakikundi mmoja alisema kwamba alilipwa shilingi 500 tu kama gharama za kutembeleana katika vikundi, ikimaanisha kwamba kuna mtu aliyeficha shilingi 6500.
* Katika kikundi kingine, ambacho tulidhani kwamba kilikuwa kinafanya vizuri, mwanakikundi mmoja alituambia kwamba alienda kununua nguo na viatu kwa ajili ya watoto, na aliombwa alete risiti feki zikionyesha gharama za juu zaidi kuliko zilizolipwa.
* Katika kikundi kingine, mahesabu yalionyesha kwamba shilingi 150,000 zilitumika kwa ajili ya taarifa ya kuja kwetu. Tunajua kwamba wafadhili wengine huhitaji kuandikwa maelezo mengi kutoka kwa wafadhiliwa wao, na hii husababisha upotevu wa fedha nyingi, na ndio maana tuliwaomba muandike taarifa ya ukurasa mmoja tu na siyo taarifa ndefu kwa Kingereza. Tulipouliza maswali, kikundi kilisema kwamba kimetumia kiasi hicho kumlipa mmoja wa viongozi wa mtandao. Kiongozi huyo alipoulizwa alikataa na kusema kwamba kiasi alichopokea ni shilingi 50,000 tu, kiasi ambacho bado ni pia kikubwa tu.
Maelelezo haya yanaonyesha tatizo moja: viongozi wengi ni waadilifu, lakini wakati mwingine kiongozi mmoja au wawili wanatafuta mbinu za kuiba fedha. Tumefikiri kwa muda murefu ni jinsi gani tutatatua tatizo hili. Ni wazi kwamba hatutaweza kulitatua tukiwa huku London na bila kuongea Kiswahili wala kuwepo Tanzania kwa mwaka mzima. Hivyo tunajaribu kuwasaidia muweze kutatua tatizo hilo. Kivipi? Kwa kuweka taratibu mpya za ruzuku mwaka huu.
Masharti ya ruzuku mpya
Kuanzia mwaka huu na kuendelea, tutaomba vikundi vikubaliane na mkataba wa Jumuiya za Afrika (AFCONET) - ahadi ya jinsi mtakavyoenenda na jinsi mtakavyotumia fedha. Awali mngeuliza kwa nini sisi huku London tunataka kuingilia shughuli za vikundi vyenu. Lengo letu ni kulinda wanachama wa vikundi vyenu, ili muwe na uhakika kwamba fedha za vikundi zinatumika kwa busara na uaminifu. Wazo kuu ni kwamba kama kikundi chenu kimesaini mkataba, basi mwenyekiti au mtunza hazina wa kikundi chenu hatawaficha chochote, na nyinyi pamoja na wananchi wengine katika wilaya yenu mtapata urahisi wa kujua kiasi cha fedha kilichoingia katika kikundi chenu na kimeenda wapi.
Maafikiano ya kuwa wazi
Mnaweza kufikiri kwamba hali hii pia ipo katika mtandao wetu. Kama mnavyojua, tunachapisha gharama za matumizi ya viongozi wetu wa mtandao katika tovuti, na daima tunawaomba ninyi muangalie na kutueleza kama mtabaini siyo sahihi. Lakini sasa tunahitaji kupiga hatua mbele. Tunataka kuweka bayana kwamba kama mwanachama yeyote wa mtandao au kiongozi ana wasiwasi au malalamiko yeyote kuhusu mtandao na jinsi unavyofanya kazi, ataweza kuwa huru kuongea na wafadhili moja kwa moja. Ni wazi kwamba hili litasababisha mabishano kama tulivyoona kwa Shabani na Jacka. Hata hivyo, hatimaye ni vema kuwa na mabishano kuliko kutunza siri-ambayo itasababisha ubadhirifu, rushwa na kufeli.
Kufanya hili litokee, tumeandaa rasimu ya 'maafikiano' ambayo tunatumaini kwamba mtandao wenu untaipigia kura kwenye mkutano kesho. Kama haya maafikiano yatapitishwa, basi tutakuwa tayari kuwalipa ruzuku mpya kwa mwaka 2008.
Ruzuku kwa ajili ya Mtandao
Kama mnavyojua, hatujatuma bado fedha nyingine kwenye mtandao kwa mwaka 2008. Hii ni kwa sababu kuna matatizo fulani fulani juu ya fedha ambazo tulizituma mwaka uliopita. Yovita Mtunza hazina wa mtandao kwa mwaka uliopita ametupatia taarifa za kutatanisha na inaonekana kwamba takribani kiasi cha shilingi 415,000 kinakosekana kwenye kiasi cha fedha ya mtandao ambacho kingetarajiwa kubaki. Labda baadhi yenu mngejiuliza, kwa nini mambo haya yatokee: je hatuviadhibu vikundi vyenu kwa kuchelewa kuwatumia fedha kwa jambo ambalo siyo kosa lenu?
Sasa ili mpate kujua kwa nini tunawafadhili, mtaona ni kwa kiasi gani mahesabu ya fedha za mtandao yalivyo muhimu. Kama mnavyojua, tunapaswa kuwaamini viongozi wa mtandao kuangalia kwamba tunatumia fedha kwa busara. Hivyo kama viongozi wenyewe hawawezi kuwajibika kwa fedha za mtandao, basi hatuwezi kuwa na uhakika kwamba wanawasaidieni ninyi kutumia fedha kwa busara. Na hatuwezi kuthibitisha kwa wafadhili wengine kwamba fedha zinatumika kwa usalama kama inavyotokea tunapozipa NGO kubwa.
Baada ya kufikiria hili kwa makini na kutmia muda masaa mengi kujaribu kupata mahesabu yaliyochanganuliwa, tumeamua kwamba suluhu iliyo na kiasi kidogo cha ubaya ni kuendelea kulipa ruzuku ya 2008 (kama maafikiano ya uwazi yatapitishwa), lakini kupunguza ruzuku kwa kiasi ambacho kimekosekana kwenye mtandao. Tunatarajia kwamba kila kikundi kitapoteza kiasi cha shilingi 20,000, lakini inawezekana kikawa zaidi au pungufu ya hapo. Kadiri iwezekanavyo, fedha itakuwa kwenye akaunti ya mtandao mwishoni mwa wiki ijayo.
Vikundi ambavyo ruzuku zao hazijapitishwa
Kutokana na tatizo ambalo nililiona wakati wa ziara yangu kwenye vikundi na kuripoti kwa jama zangu huku London, tumebainisha vikundi vitatu ambavyo ruzuku zao za 2008 hatujapitisha. Navyo ni:
* PHCF, kwa sababu tunasubiri kuona uthibitisho wa jinsi fedha zilivyotumika kwa mwaka 2007
* CISO, kwa sababu mfadhili mwingine alitoa malalamiko jinsi fedha yao ilivyotumika na tungependa kujua matokeao yake kabla hatujafanya uamuzi wa ruzuku yetu
* Chiyowonet, kwa sababu mfadhili mwingine alitoa malalamiko juu ya fedha yao ilivyotumika na tungependa kujua matokeo yake kabla hatujafanya uamuzi wa ruzuku yetu
Uanachama wao kwenye mtandao umesitishwa kwa kipindi hiki, hivyo hawatapaswa kuhudhuria mikutano ya mtandao na hamupaswi kutumia fedha za mtandao kulipwa kwa kufanya ziara kwao. Tutawajulisha baadae kama kutakuwa na mabadiliko yeyote yale, na ndipo kikundi chochote kati ya hivyo kinaweza kujiunga tena na mtandao.
Vikundi ambvyo vitapokea ruzuku ya vitu
Kwa baadhi ya vikundi, tumeona dalili kwamba kikundi kina ujunzi hafifu katika kutunza na kutumia fedha, na hivyo tumeamua kuwapa ruzuku kwa njia ya neti za mbu na siyo fedha tasilimu. Watazigawa neti hizo kwa watoto walio katika mazingira magumu jirani, na kama watafanya hivyo kwa ufanisi, basi watakuwa na haki ya kupokea ruzuku ya fedha tasilimu baadae. Vikundi hivyo ni:
* Moms in Touch
* Twafaha
* Woyona
Vikundi vitakvyopata ruzuku kwa awamu (roborobo)
Kwa baadhi ya vikundi, tuliona kwamba kikundi kinafanya kazi nzuri, lakini tunawasiwasi kwamba kuna hatari kwamba mtu mmoja au wawili wanafanya uamuzi wa kila kitu na kwamba kuna mazingira hatari kwamba fedha inaweza isitumike vizuri. Kwa vikundi hivi, tumeamua kuwapa robo ya ruzuku ya mwaka na kuwaomba waimarishe uongozi. Kama watafanikiwa kufanya hili, tunatumaini kwamba baadae wataweza kupokea ruzuku kwa mwaka na siyo kwa awamu ya robo. Vikundi hivyo ni:
* Red House
* Tawosu
* Wolisu
Kama mnavyojua, vikundi vyenu vyote vinasaidia watoto ambao wako katika mazingira magumu zaidi. Daima uamuzi huu wa kupunguza au kuweka masharti ya ruzuku kwa vikundi huwa mgumu sana. Kadhalika, tunapaswa kuzingatia kwamba haya yote tunayafanya kwa ajili ya kusaidia watoto – na kwamba hatimaye tutaweza kusaidia watoto wa Dar es Salaam zaidi kama tutatoa fedha kwa vikundi ambavyo vina mpango mzuri, uaminifu na uwazi kuliko vile vinavyopungukiwa na hayo.
Kwa niaba ya wenzangu haku London, napenda kuwatakieni ninyi nyote pamoja na watoto mnaowasaidia mwaka 2008 wenye mafanikio mema.
kila la heri
Tim
Imetafsiriwa na
Donatian Marusu
Mratibu
26/01/2008
Maafikiano ya kuwa wazi
Mtandao wa Jumuiya za Afrika, Dar es Salaam
Sisi, wanachama wa mtandao wa jumuiya za Afrika, tunaamini kwamba kwa matashi mema ya watoto tunaowasaidia, matatizo kwenya mtandao wetu sharti yabainishwe, yajadiliwe na wote na kutatuliwa. Ili kutimiza haya, tumepigia kura sera rasmi za mtandao wetu zifuatazo:
1. wanachama wote wa vikundi ndani ya mtandao, na viongozi na waratibu wote wa mtandao watakuwa huru kuwasiliana na kiongozi yeyote wa kikundi chochote kile ndani ya mtandao na kukabidhi taarifa yeyote ile au maoni wanayodhani ni sahihi.
2. Wanachama wote wa vikundi ndani ya mtandao, na viongozi na waratibu wote wa mtandao watakuwa huru kuwasiliana na wafadhili wa vikundi au wa mtandao na kukabidhi taarifa yeyote ile au maoni wanayodhani ni sahihi.
3. Ingawa matatizo yanaweza kushughulikiwa kwa haraka kwa majadiliano na viongozi wa mtandao au viongozi wa vikundi na kwa upole na kwa kujali vinaweza kufanya zoezi la kutatua matatizo liwe rahisi, hakuna wanachama wa vikundi ndani ya mtandao au viongozi au waratibu wa mtandao watastahili kuaadhibiwa au kuadibishwa kwa kutoa taarifa kwa mfadhili, kiongozi au wanachama wa kikundi, hata kama tarifa hiyo ni ya kweli au siyo.
Zingatia: maafikiano yanapaswa kupitishwa kwa wingi wa kura za wapiga kura waliopo mkutanoni kabla shirika letu halijaamua kutoa ruzuku ya 2008.
1

Comments